Thursday 1 December 2016

MADINI ya Makaa ya Mawe (Coal Mines) Tanzania

Nchi yetu ni tajiri mkubwa wa madini mbali mbali yakiwemo madini ya MAKAA YA MAWE.

Makaa ya mawe ni nini?

Makaa mawe ni aina ya mwamba mashapo au mwamba metamofia na fueli kisukuu muhimu. Ilitokea kutokana na mabaki ya mimea ya kale iliyogeuzwa kuwa aina ya mwamba katika mchakato wa miaka mamilioni.
Kikemia ni hasa kaboni. Kijiolojia inatokea kama kanda pana au nyembamba katikati ya miamba mengine. Huchimbwa mara nyingi katika migodi chini ya ardhi au kama iko karibu na uso wa ardi katika machimbo ya wazi yaliyo kama mashimo makubwa.




Katika nchi yetu madini haya yanapatikana maeneo ya fuatayo (kwa sasa):-

-KIWIRA
-LUDEWA
-RUVUMA
-MBINGA
-SONGEA

UTAFITI umebaini kuwa madini ya makaa ya mawe ambayo yanachimbwa kwenye Mgodi wa Ngaka, wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma yanaongoza kwa ubora duniani. Kabla ya kuanza rasmi mgodi huo, taarifa zinaonesha kwamba zaidi ya tani 1,000 za makaa ya mawe zilisafirishwa kupelekwa nchini Afrika ya Kusini ili kuchunguza ubora wa madini hayo.
Matokeo ya utafiti huo uliofanyika kuanzia mwaka 2008 umeonesha kuwa ubora wa madini hayo haufanani na madini ya makaa ya mawe yanayochimbwa katika nchi yoyote duniani. Utafiti umebaini kuwa mgodi huo unakadiriwa kuwa na zaidi ya tani milioni 400 za makaa ya mawe.
Kiasi hicho, kwa mujibu wa wataalamu waliofanya utafiti, kinaweza kuchimbwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 100. Utafiti wa madini hayo ulifanyika kwa kuangalia wingi wa madini ya makaa wa mawe, unene wa mwamba na ubora wa makaa hayo. Utafiti umebaini kuwa kijiji cha Ntunduwaro kipo juu ya mwamba bora wa madini ya makaa ya mawe ambayo yamesambaa pia na maeneo jirani ya kata ya Ruanda.
Mkuu wa Masoko wa Mgodi wa Ngaka, Christopher Temba anasema mgodi huo unazalisha tani za makaa ya mawe laki tano kwa mwaka lakini lengo ni kufikia tani milioni moja. Madini hayo yanasafirishwa katika nchi za Kenya, Zambia na Malawi.
Mgodi wa Ngaka, unamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye asilimia 30, na Kampuni ya Intra Energy ya Australia yenye hisa ya asilimia 70.
Kulingana na Kaimu Meneja Mkuu Uzalishaji wa Kampuni ya TANCOAL, Boscow Mabena, kampuni hiyo kuanzia Julai 2014 hadi Desemba 2015 imezalisha tani 272,852 za makaa ya mawe na kati ya hizo, tani 257,570 zimeuzwa na kuwezesha Serikali ya Tanzania kuingiza fedha kwa kodi zaidi ya Sh bilioni 2.
Mabena anawataja wateja wakuu wa madini hayo hapa nchini kuwa ni viwanda vya Lake Cement, Tanga Cement, Mbeya Cement, Dangote, Mufindi Paper Mills na Mohamed Interprises.
Anasema, awali viwanda hivyo vilikuwa vinaagiza madini ya makaa ya mawe toka nchini Afrika ya Kusini jambo lililosababisha gharama kuwa juu huku serikali ikikosa mapato.
Anabainisha kuwa Kampuni ya TANCOAL imepewa vitalu saba vya kuchimba madini ya makaa ya mawe ambapo kila kimoja kina ukubwa wa kilomita za mraba 9.9 na shughuli ya uchimbaji katika mgodi huo imetimiza miaka mitano hadi kufikia mwaka 2015.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Ntunduwaro, John Haule, Agatha Mapunda na Mary Komba wanatoa rai kwa serikali kuhakikisha madini hayo yanawanufaisha Watanzania na kuinua uchumi wa taifa. Wanaiomba Wizara ya Nishati na Madini kusimamia rasilimali hiyo kwa mujibu wa sera na sheria zilizopo ili Watanzania wanufaike kwanza badala ya wageni kupata manufaa zaidi.
Lakini pia wameonya kwamba kama una madhara ya kiafya wanayopata wananchi wanaozunguka mgodi yasifumbiwe macho bali itafutwe njia za kuyaondoa.
Kwa upande, wake serikali imesema itahakikisha mgodi wa madini ya Makaa ya Mawe ya Ngaka unakuwa chanzo kingine muhimu cha uzalishaji umeme nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyasema hayo mapema mwaka huu alipotembelea Mgodi wa Ngaka ambao hisa za Serikali zinawakilishwa na Shirika la NDC.
Ili kufikia lengo hilo, Waziri Muhongo anasema serikali itahakikisha inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na mgodi huo.
Ameagiza wadau muhimu wa madini hayo ambao ni Kampuni ya TANCOAL, NDC, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, na wananchi wanaozunguka mgodi kukutana ili kujadili na kukubaliana kuhusu masuala kadhaa yakiwemo fidia na uhifadhi wa mazingira.
Profesa Muhongo amevitaka viwanda vilivyoingia mkataba wa mauziano na mgodi huo kuacha kununua madini hayo kutoka nje kwa kuwa makaa ya mawe ya Ngaka yanakidhi viwango na ubora unaotakiwa.
“Nimeelezwa makaa ya Ngaka yana ubora na kiwango cha hali ya juu na nimeelezwa kwamba kuna baadhi ya viwanda vimeingia mkataba na Ngaka, lazima tutumie bidhaa za nyumbani,” anasisitiza Profesa Muhongo.
Anasema ni muhimu kutumia makaa ya mawe kuzalishia umeme kwa sababu gharama zake ni nafuu kwa wananchi na pia umeme huo utachochea ukuaji wa viwanda nchini.
Licha ya madini ya makaa ya mawe kulalamikiwa kuchafua mazingira duniani kote, utafiti umebaini kuwa umeme unaotokana na madini hayo ndio unaotegemewa zaidi na mataifa mengi yaliyoendelea duniani.
Takwimu zinaonesha kuwa makaa ya mawe yanachangia asilimia 41 ya umeme unaozalishwa duniani, umeme wa maji asilimia 16, umeme wa gesi asilia asilimia 20, nyuklia asilimia 15 na umeme wa mafuta kwa kutumia jenereta ni asilimia sita tu kutokana na kuwa umeme ghali.
Utafiti umebaini kwamba miongoni mwa mataifa yaliyoendelea kiuchumi duniani ni yale ambayo yanatumia umeme wa makaa ya mawe.
Mataifa hayo ni pamoja na Afrika Kusini inayotumia asilimia 93 ya umeme wa makaa ya mawe, Poland asilimia 92 na China asilimia 79. Nchi nyingine ni Australia asilimia 77, Kazakhstan asilimia 70, India asilimia 69, Israel asilimia 63, Jamhuri ya Czech asilimia 60, Morocco asilimia 55, Ugiriki asilimia 52, Marekani asilimia 49 na Ujerumani asilimia 46.
Katika kutekeleza Dira ya Taifa ya mwaka 2025 Tanzania inatarajia kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ambayo yameenea katika mikoa ya kusini, hususan mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Iringa na Njombe.
Sera Taifa ya Madini ya mwaka 1997 inasisitiza juu ya sekta binafsi kuendeleza madini ambapo serikali katika sera hiyo ina jukumu la kuidhibiti, kuikuza na kuiendeleza sekta hiyo.

Chanzo: http://www.habarileo.co.tz/index.php/makala/16227-makaa-ya-mawe-ya-tanzania-bora-zaidi-duniani


1 comment:

Unknown said...

uzi mzuri, na je mtu binafsi nikitaka nifanye huu uchimbaji kama kampuni yangu wateja hawasumbui upatikanji wao. hmna soko lingine la nje.